Dishon Amanya – Bungoma
Mwezi mzima wa Agosti baada ya mwaka mmoja, Jamii ya Wabukusu moja kati ya jamii ya Waluhya husherehekea sherehe maalum ya kuwapasha vijana Tohara kama njia moja ya kuvuka kwenye utu uzima.
Sherehe hizi huchukuliwa kwa uzito mkali kwani ndio mojawapo ya mila na desturi za wabukusu zilizothaminiwa sana maeneo ya kaunti ya Bungoma, Trans-Nzoia na hata sehemu kadhaa nchi jirani ya Uganda.
Safari yetu ya kupata kila mchakato wa sherehe hizi ilianza mida ya saa kumi tulipoungana na kijana ambaye alikuwa anatarajia kupashwa tohara siku itakayofuata.
Usiku mzima tulikaa kwenye vibao na wazee wa jamii ya Wabukusu huku wakitusimulia kila hatua itakayofanyika kabla ya kijana kuukabili kisu cha ngariba.
Katika kijiji cha Bwake eneo Bunge la Kabuchai, Kaunti ya Bungoma, wakati huo kijana tayari amewasili katika Kijiji chake kutoka kwa mjomba wake, akiwa na ng’ombe, na kama mzee wa kijiji anavyosimulia hio ni mojawapo ya hatua muhimu sana katika sherehe hizi za tohara.
“Kwenda kwa mjomba ni sehemu muhimu katika tamaduni hii ya upashaji tohara, kule mambo kadhaa hufanyika mojwapo ikiwa ni kupewa mawaidha na mjomba na hatimaye kuzawadiwa ng’ombe.” Mzee asimulia.
Aidha, anadokeza kuwa kulingana na umbali wa sehemu mjomba anaishi kijana huandamana na umati wa watu kama mashuhuda na ndio watakaomwingiza nyumbani kwao kutoka kwa mjomba.
“Ng’ombe huyu ni zawadi kutoka kwa mjomba , baraka maalum kwa ajili ya sherehe inayosubiriwa, na hii hutokea tu ikiwa baba alilipa mahari kwa wakwe,” Mzee aliongezea.
Nyumbani kwao, Babake na jamii wanampokea, Mamake anamkaribisha kwa shangwe na nderemo, umati wa watu wakiwemo majirani, ukoo na marafiki za kijana wanafurika kwenye boma hilo.
Nyumbani ,baba anamtia hofu mwanawe kwa ukali wa kisu kinachomsubiri kwa kumnyang’anya Kengele zinazofahamika kama chinyimba, kijana anahuruhusiwa kupata pumziko na kupata lishe kujiandaa kwa mchakato mzima wa khuminya kuanzia saa nne hadi saa saba za usiku.
“Wakati huu wote kijana analindwa kama rais na mlinzi kokote anakoenda ata msalani anasindikizwa kwa ulinzi mkubwa.” mzee anaeleza.
Kuwa kijana rijali kwa jamii hii ya wabukusu lazima upitie hatua nyingi na mambo ambayo hufanyiwa unaweza ukakata tamaa ila kuzuia aibu ya kuogopa kisu hicho kijana hupewa ulinzi mkali ili asiaibishe jamii hiyo.
Muda wote huu wa Khuminya Usiku, kikundi cha Babake almaarufu age set (Bakoki) wamezunguka kichungu hiki kila mmoja na mrija wanafurahia pombe ya kienyeji aina ya Busaa ndani ya nyumba, katika kikao hiki wazee huendeleza gumzo huku wakifurahia, ni katika kikao hiki ambapo wazee hukumbushana baadhi ya mila na desturi zao, huku wakirekebishana pale walipoenda kinyume na mila.
Saa nane asubuhi, Kijana anaruhusiwa kupumzika tena kwa muda usiozidi masaa kulingana na umbali wa mto atakaopelekwa, kijana hutandikiwa mkeka mara nyingi matawi ya ndizi hutumika ili kijana aweze kupata lepe la usingizi kabla ya siku hiyo.
Muda wote huo wa usiku wazee huendelea kunywa busaa huku watu wengine wakiendelea kuimba wakati vijana hawa wamepelekwa chumbani kupumzika,” Anadokeza.
Saa kumi na mbili alfajiri Kijana yuko tayari kupelekwa mtoni ,tena kwa maonyo mengi ikiwa anaogopa kujisalimisha, lakini hayo yote hayamzuii kuukabili kisu cha ngariba.
Mtoni, Kijana anapakwa matope mwili mzima na Mjomba wake, jamaa yake wa karibu au hata jirani, wote hawa lazima wawe na tabia njema katika jamii.
Juu ya kichwa chake nyasi huwekwa, kwa jadi inamaanisha kuwaunganishwa na mababu.
Baada ya hapo ,ni wakati wa kuelekea nyumbani. Huku wakiimba nyimbo za Sioyayoo, wimbo maalum ambayo huimbwa baada ya kijana kutoka mtoni.
Wakati huu baada ya mchakato wote hakuna nafasi ya kukwepa kisu, kwani wao huamini ni lazima ukakutane na kisu cha ngariba liwe liwalo.
Punde tu kijana anawasili kuna sehemu ambapo mmoja wa jamaa zake hukutana nae akiwa amebeba mwiko, kulingana na sheria za tamaduni yao, kijana anastahili kuukwepa kulamba mwiko huo, hivyo basi anapaswa kuwa makini sana ili asivunje sheria hio.
Kule nyumbani, baba anamngoja mwanawe Kwa mshikamano kwa ajili ya mpito, anamchukua na kumsindikiza hadi kwenye jukwaa linalojulikana kama etiang’i, sehemu ambayo shughuli hio hufanyika.
Wakati huu mama yuko pamoja na wanawake wengine chini kwenye sakafu kwa Nyumba wakimwombea mtoto wao.
Mlio wa filimbi sekunde chache baadae inaashiria kuwa kazi imekamilika, mamake anaongoza Vigelegele kutoka kwa nyumba.
Kijana anaketishwa na kuzawadiwa,dada mdogo kwa kipindi chote cha uponyaji atakuwa msaada wake, anamtoa tope kichwani.
Kijana anapelekwa kwa nyumba kinyume nyume baada ya kuzungushwa ,kulingana na wazee inaashiria sasa amevua nguo ya mama na amevalia nguo ya baba kirasmi .
Kijana huyu atakuwa kwenye chumba cha faragha kinachojulikana kama mwikombe kwa muda wote kwa ajili ya uponyaji hadi mwezi Disemba atakapotoka rasmi katika hafla maalum iitwayo khukhwiyalula.