Dishon Amanya-Bungoma
Takwimu za hivi punde kutoka kwa Baraza la Kitaifa la Kudhibiti Magonjwa ya SDCC zimefichua kuwa vijana wenye umri kati ya miaka 13 na 35 sasa wanachangia asilimia 75 ya maambukizi mapya ya VVU.
Akizungumza wakati wa hafla ya uhamasishaji wa wanafunzi katika shule ya Sekondari ya Matili huko Kimilili, Douglas Bosire anayesimamia takwimu katika idara hiyo alisema mengi ya maambukizi mapya yanatokana na idadi kubwa ya unyanyasaji wa kijinsia dhidi ya vijana.
“Takwimu zinatia wasiwasi na kuna kitu kinahitajika kufanywa haraka ili kuokoa watoto wetu,” alisema.
Bosire anadokeza Kaunti ya Bungoma ilirekodi jumla ya mimba za utotoni 11,713 mwaka wa 2023, ikiwa ni asilimia 21, kile anachosema kimeimarika kidogo hadi 19%, hata hivyo, akisisitiza kuwa takwimu bado zinatia wasiwasi.
“Hii inarudisha nyuma maendeleo ya masomo yao kwani wengi wao hulazimika kuacha shule kwa muda au hata kabisa ili wawatunze watoto wao,” aliongeza.
Kongamano hilo la uhamasishaji lilihudhuriwa na seneta mteule Catherine Mumma ambaye amechukua hatua ya kuwaelimisha vijana dhidi ya tishio hilo la Triple Threat.
“Huu ni mpango ambao tumeuchukua kama viongozi ili kurejesha heshima ya vizazi vyetu vijavyo vilivyo hatarini kutoweka, watu wote wenye mawazo kama hayo wanapaswa kujitokeza kwa ajili ya watoto wetu wa kiume na wa kike,” alisema.
Aidha, anadokeza ni wakati muafaka kwa wasichana wadogo kuanza kupata Elimu ya Afya ya Uzazi ili waendelee kufahamu hatari zinazowakabili kujihusisha mapema katika shughuli za uzazi.
Nae Mwakilishi wa wanawake kaunti ya Bungoma Catherine Wambilianga alitumia fursa hiyo kuthibitisha kuwa wabunge katika Bunge la Kitaifa na Seneti wanafaa kutunga sheria zinazofaa ili serikali iweze kutoa visodo kwa shule zote ili kuhakikisha wasichana wanaotoka katika familia zisizojiweza wananufaika.
Tishio hilo la Triple threat linajumuisha maambukizi mapya ya VVU, Mimba za utotoni na Ukatili wa Kijinsia, jambo ambalo Baraza la Taifa la Kudhibiti Magonjwa limeahidi kupambana nalo kwa kuwahusisha washikadau mbalimbali.